Sunday, August 5, 2012

Dar es Salaam: Askari, Wanamgambo washikiliwa kwa tuhuma za wizi wakitumia silahaASKARI wa Jeshi la Polisi kituo cha Mbagala, mwenye namba E 995 Koplo Robert (40), mkazi wa Kitunda, Dar es Salaam anashikiliwa kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha.

Habari za uhakika zilizopatikana ndani ya jeshi hilo jana, zilidai kuwa Robert anashikiliwa pamoja na wanamgambo wawili, MG 505002 Bundala Magesa (48) na MG 558537 Ibrahim Majula (45).

Ilidaiwa kuwa Agosti 3 saa 8 usiku maeneo ya Mikwambe, Mbagala wilayani Temeke, askari huyo pamoja na mgambo watatu akiwamo mwingine Ramadhan (marehemu) ambaye ubini wake haukujulikana mara moja, waliiba vitu mbalimbali nyumbani kwa Fadhili Said.

Habari ziliendelea kudai kuwa vilivyoibwa ni chaja sita za simu, headphone moja, vifaa vya kuchomelea simu viwili, spana moja ya gari, kipimajoto kimoja na mkoba mdogo wa rangi ya pinki vikiwa ndani ya gari la askari huyo lenye namba T 106 BET aina ya Toyota Corolla rangi nyeusi.

Hata hivyo kikisimulia tukio hilo, kilidai kuwa siku hiyo, askari huyo aliwafuata mgambo hao na kuwataka kwenda Mikwambe katika nyumba ya mkazi mmoja wa eneo hilo kwa lengo la kuiba ng’ombe wake wanane.

Ilidaiwa kuwa walipokaribia eneo hilo, walifyatua baruti, wakati kikosi cha Ulinzi Shirikishi Jamii kikijiandaa kwenda kuanza doria na hivyo kikajipanga na kuwazingira askari hao, lakini wawili wakakimbia na kukamatwa baadaye.

Lakini wakati wakikimbia, mmoja alikamatwa na walinzi hao na kumshambulia wakamwua na kumchoma moto, huyo ndiye aliyetambuliwa kwa jina moja la Ramadhani.

Ilidaiwa kuwa Koplo Robert alipobanwa alijitambulisha kuwa ni askari polisi wa kituo cha Mbagala na ndipo uongozi wa kikosi hicho cha ulinzi shirikishi ulipowasiliana na viongozi wa kituo hicho ambao walifika eneo hilo na kumtambua kuwa ni askari wao.

Chanzo hicho kililiambia gazeti hili, kwamba baada ya waliokimbia kukamatwa na kubaini mwenzao ameuawa, waliamua kuweka kila kitu hadharani, wakimtuhumu Koplo Robert kuwa ndiye aliyewapeleka huko.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, jalada namba MBL/RB/7431/12 limefunguliwa Mbagala kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, David Msime alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, aliomba kupewa muda wa kufuatilia, akiahidi atafutwe baada ya nusu saa lakini hakuweza kupatikana tena kwa simu, kwani mara zote iliita bila ya kupokewa.

via HabariLeo
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!