Wednesday, August 15, 2012

"NITAANIKA KILA KITU BAADA YA SIKU 40 KUANZIA SASA.".......DKR ULIMBOKA


MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt. Stephen Ulimboka, amesema anatarajia kuanika madudu ya watu waliomteka na kumfanyia vitendo vya kinyama, baada ya kufanya uchambuzi wa kina mkasa uliomkumba.

Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dkt. Ulimboka alisema ataanika madudu yote aliyofanyiwa, baada ya siku 40.

Dkt. Ulimboka, aliyerejea kutoka nchini Afrika Kusini, alikokuwa amekwenda kutibiwa, alisema ana siri nzito moyoni ambayo akiitoa, Watanzania watamuelewa tu.

Alisema baada ya kurudi nyumbani salama, hivi sasa amejikita zaidi kufanya uchambuzi wa mambo au matukio yaliyomsibu kabla ya kupelekwa Afrika Kusini ili ukweli ujulikane.

“Nawaomba Watanzania wawe na subira kwanza, nitaanika kila kitu baada ya siku 40 kuanzia sasa, jambo kubwa ninaloangalia sasa ni kuimarisha kwanza afya yangu ambayo Mungu amenipigania vya kutosha, baada ya hapo nitaeleza kwa kina mkasa huu ulionikuta wakati wa mapambano ambayo nyote mnayajua. 


Napenda kuwahakikishia Watanzania na madaktari wenzangu, kuwa nitaendelea kusimamia kile ninachoamini na kukitetea…nitaendelea kuongoza Jumuiya ya madaktari, nitaendelea kujiamini ili kuhakikisha tunapigania madai yetu,” alisema Dkt. Ulimboka.

Kuhusu familia yake, kama inaweza kutoa tamko, Dkt. Ulimboka alisema hafahamu iwapo familia imeandaa mpango huo, lakini kwa upande wake, wakati ukifika atalitoa mbele ya umma kama ilivyo kawaida yake kwa ushahidi wa kutosha.


 “Kuhusu suala la uchunguzi, siwezi kulizungumzia sana kwa sababu kama nilivyosema siwezi kukurupuka kuanza kutoa ushirikiano na Jeshi la Polisi, wakati sijausoma mkasa wenyewe kama unaendelea vipi. 

Nimesikia baadhi ya vyombo vya habari, vikisema nimefichwa, jamani sijafichwa na familia…. naendelea na shughuli zangu kama kawaida, lakini jambo la msingi ni kuimarisha kwanza afya yangu, kabla ya kuanza kukutana na waandishi wa habari hadharani,” alisema Dk. Ulimboka na kuongeza, “Nipo kwenye mihangaiko yangu na muda huu nipo safarini, naelekea mjini Bagamoyo.”

Katika hatua ya kushangaza, Dkt. Ulimboka aliamua kutumia usafiri wa boti kwenda Bagamoyo, tofauti na siku ambazo amekuwa akitumia njia ya barabara.

Hii ni mara ya kwanza Dk. Ulimboka kuzungumza kwa kina na MTANZANIA, tangu aliporejea kutoka nchini Afrika Kusini, ambako alikwenda kutibiwa Juni 27, mwaka huu.

Wakati Dkt. Ulimboka akisema hayo, ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi nchini, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliiambia MTANZANIA kuwa, hivi sasa jeshi hilo linaendelea na vikao ili kuona ni namna gani wanaweza kushughulikia suala la Dkt. Ulimboka.

Habari za kuaminika kutoka kwa ofisa huyo, ni kwamba Ijumaa wiki hii linaweza kutoa ufafanuzi zaidi au hatua zitakazochukuliwa dhidi ya daktari huyo.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!