Wednesday, August 1, 2012

Kwa migomo hii, Serikali ijitathmini jinsi mgawanyo wa keki ya Taifa ulivyo kwa wote

Wakati wananchi wakiendelea kutafakari athari za mgomo wa madaktari uliofanyika mwezi uliopita na kuishia kwa tukio la kutisha la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, jana taifa limeanza tena kushuhudia machungu ya mgomo wa walimu uliotangazwa na Chama cha Walimu (CWT). 
Picture
Kwa mujibu wa CWT mgomo huo ambao serikali inadai ni batili kwa kuwa umefikiwa bila kufuata taratibu za kisheria, unahusu madai ya walimu ya nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia ya asilimia 50 ya mshahara na posho ya mazingira magumu ya asilimia 30, mambo ambayo yanaelezwa kuwa serikali imeshindwa kuyajadili kwa kuwa kumekuwa na mgogoro na walimu.

Kutokana na mgomo huo usio na ukomo, jana huduma za masomo katika shule nyingi nchini zilivurugika kwa kuwa baadhi ya walimu ama hawakwenda kabisa kazini au waliokwenda hawakufundisha kwa maana hiyo kuwafanya wanafunzi kukosa masomo.

Jana suala hilo pia liliibuka bungeni kwa baadhi ya wabunge kutaka kusikia tamko la serikali juu ya mgomo wa walimu, lakini kiti kilisema kuwa kwa mujibu wa taarifa zilizoko ni kwamba kuna kesi kati ya walimu na serikali iliyoko mahakamani na pande zote mbili zinatakiwa kuwasilisha maelezo yake leo.

Serikali inasema kuwa imekwenda mahakamani baada ya kushindwa kufikia makubaliano na walimu katika Tume ya Maridhiano (CMA), hivyo kutafuta haki mahakamani.

Tunasikitika kwamba katika siku za hivi karibuni utaratibu wa kutatua matatizo ya watumishi wa umma na serikali umekuwa ni wa migomo. Hali hii imekuwa na matokeo hasi kwa wananchi kwa sababu wanakosa huduma kutokana na migomo hiyo, kama ilivyokuwa kwa mgomo wa kwanza wa madaktari Februari mwaka huu na hata huu wa Juni pia, watu wengi wamekufa na wengine kupata madhara mengine makubwa.

Kimsingi hatuungi mkono migomo kama njia ya kutatua matatizo ya wafanyakazi, kwa sababu kwa kutumia njia hiyo madhara yamekuwa ni makubwa kwa wananchi moja kwa moja, lakini pia hata hao wanaogoma mahusiano na waajiri wao (serikali) yameathirika pia kiasi cha kukosekana kwa hali ya kuaminiana.

Kadhalika, tunafikiri kuwa njia ambayo serikali imekuwa ikitumia kwa kukimbilia mahakamani ama kusitisha migomo ambayo tayari imekwisha kuanza au kuzuia kuanza kwa mgomo, nayo pia siyo nzuri kwa sababu mbali ya kujenga picha kuwa haki za wafanyakazi kwa njia fulani zinakiukwa pia inatoa taswira kuwa serikali imekuwa haichukulii kwa uzito unaostahili majadiliano na watumishi wake kwa kuwa inajua kuna upenyo wa mahakama.

Sisi tunaamini kwamba mazunguzo yenye nia ya kweli katika kufikiwa kwa makubaliano ndiyo njia pekee ya kujenga maelewano na kuaminiana baina ya serikali na watumishi wake katika sekta zote.

Tunajua kuna nyakati watumishi wa umma wanadai mambo ambayo ni magumu kutekelezwa kama yalivyo, lakini ukubwa wa madai hayo siyo hoja kama serikali itakubali kukaa kitako kuzungumza na kujenga hoja za msingi juu ya kwa nini kwa mfano ni  vigumu kutimizwa kwa madai makubwa yanayowasilishwa kulingana na uwezo wa kiuchumi wa taifa.

Wakati tukieleza masikitiko yetu juu ya athari za migomo ya watumishi wa umma kwa wananchi wanaohudumiwa, tungependa pia serikali ikajiuliza maswali magumu juu ya mwenendo huu wa mfululizo wa migomo ya watumishi wake kwamba ni kwa nini imekuwa mingi katika kipindi hiki kuliko huko tulikotoka? Je, kuna tatizo la mawasiliano? Je, kuna nini hasa kipya kimetokea kiasi cha kuwafanya watumishi wa umma sasa waamue tu kuwa migogoro dhidi ya mwajiri wao ndiyo njia pekee ya kupata wakitakacho.

Kujitazama huku ni pamoja na serikali kufanya tathmini ya kina juu keki ya taifa inavyogawanywa. Je, kuna usawa na haki jinsi makundi mbalimbali katika jamii yanavyonufaika na kesi hiyo; je, kila mmoja anajiona akijaliwa katika mgawanyo huo? Inawezekana ni dhana tu imejengeka au ni kweli pia kuwa kuna kundi moja katika jamii linalonufaika zaidi na keki hiyo huku wengine ndani ya jamii wakati wavuja jasho wakuu wakiaambulia sehemu ndogo sana.

Kwa maneno mengine migomo hii ni lazima sasa iiamshe serikali na kujitathmini kwa mapana yake jinsi mgawanyo wa keki ya taifa unavyofanyika kwa haki miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii, bila kutazama hili migomo inaweza kuongeza zaidi na kuleta athari kubwa zaidi za kijamii kwa taifa letu.

via NIPASHE
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!