Friday, August 3, 2012

LISSU,MUHONGO KUTOA USHAHIDI WA RUSHWA


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ameunda kamati ndogo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuchunguza tuhuma za wabunge kuhongwa, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akitajwa kuwa mmoja wa watakaolazimika kwenda kutoa ushahidi.

Mbali na kuunda kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi (CCM), pia ameipa Kamati hiyo hadidu za rejea na muda wa wiki mbili kukamilisha kazi hiyo.
“Baada ya kushauriana, imeonekana suala hili litafanyika vizuri kwa kuunda kamati ndogo ya wabunge watano ili ifanye haraka, kazi itafanyika kwa wiki mbili na taarifa itawasilishwa kwa Spika,” alisema Spika Makinda.

Kamati hiyo kuwa ni pamoja na kukutana na kukubaliana namna bora ya kufanya kazi na mapendekezo, kwa kuzingatia misingi ya haki ya asili. Pia kupitia taarifa rasmi za Bunge za siku za mjadala wa makadirio ya Bajeti ya Nishati na Madini ili kujiridhisha kuhusu mjadala ulivyoendeshwa.

Pia imetakiwa kuita mashahidi akiwamo Mnadhimu Mkuu Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu ambaye alitaja baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa, akidai kuwa walikuwa na mgongano wa maslahi katika suala hilo.

Wengine ni Profesa Muhongo ambaye alitoa tuhuma za baadhi ya wabunge kuhongwa na kuwa na maslahi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wakati wa majumuisho yake.
Pia itaita wabunge wote waliochangia makadirio ya Bajeti hiyo na kutoa tuhuma kuhusu wenzao kuhongwa na mbunge yeyote anayeweza kutoa ushahidi.

Wajumbe mbali na Ngwilizi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wajumbe wengine ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Omar Juma (CUF), Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (Chadema) na wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM).

Wajumbe wote wa kamati hiyo ni wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na uteuzi wao ulifanywa na Spika kwa kushauriana na Ngwilizi.

Hatua hiyo ilitangazwa jana baada ya baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kusema baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hawawezi kutenda haki.

Mbatia alisema hayo akibainisha kuwa baadhi ya wajumbe hao wanatokana na Kamati ya Nishati na Madini, iliyovunjwa na Spika, baada ya kutuhumiwa kwa rushwa ili wawajibishe viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, hasa Profesa Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi.

Kati ya wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, waliokuwa katika Kamati ya Nishati na Madini, aliyekuwa katika kamati zote ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM).

Sendeka alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na kutakiwa kuchunguzwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambako mbunge huyo pia ni Makamu Mwenyekiti. Hata hivyo, katika uteuzi wa jana, Sendeka hayumo.

Wabunge wengine ambao ni wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambao hawamo katika kamati ndogo ni Mbunge wa Tumbe, Rashid Ally Abdallah (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Maua Daftari (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christine Ishengoma (CCM) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi).

Wengine ni Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), ambaye alitoa hoja ya kuvunjwa kwa Kamati ya Nishati na Madini, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema); wa Mbogwe, Augustino Masele (CCM); wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP); wa Viti Maalumu, Cynthia Ngoye (CCM) na wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), NCCR wampinga Blandes Baada ya Spika Makinda kutangaza wajumbe wa kamati ndogo ya Bunge jana, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisimama baadaye kuomba Mwongozo.

Alipopewa nafasi alisema Kamati hiyo ina wajumbe wengi wa CCM, hivyo imekosa uwiano wa vyama vya upinzani. Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali ambaye hata hivyo alikataliwa kuomba Mwongozo kwa kuwa ulihusu jambo moja.

Akitoa Mwongozo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama alisema Spika alitoa uhuru kwa mbunge yeyote kwenda kuisaidia Kamati, ikiwamo kupinga wajumbe wa Kamati hiyo na isingewezekana kila mmoja kuwa katika Kamati hiyo.

Baada ya hapo, Machali aliandika barua na kuweka kielelezo kwa Spika akipinga uteuzi wa Blandes kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa wabunge waliopinga uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini wa kuipa zabuni ya kununua mafuta ya IPTL, kampuni ya Puma Energy.

Hata hivyo, hakuna aliyempinga Arfi ambaye juzi wakati Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), akijibu tuhuma dhidi yake kuwa alihongwa, alifuatana na Arfi kama mmoja wa wabunge wanaomwunga mkono.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!