Thursday, August 2, 2012

Mahojiano Rasmi na Bondia Mtanzania Aliyedundwa na Kutolewa Kwa Pointi 20 Dhidi ya Zake 7 Kwenye Mashindano Ya Olimpiki ya 2012.

Bila shaka masikio na macho ya Watanzania wote yamekuwa yakiumizwa na kushindwa tayari kwa wanamichezo wetu watatu waliokuja hapa London kushiriki Olimpiki ya 2012.

Waogeleaji wawili, Ammaar Ghadiyali (miaka 15) na Magdalena Moshi (21) walitolewa  raundi ya kwanza ya uogeleaji, juzi Jumanne na Jumatano. Wa mwanzo lakini alikuwa bondia Selemani Kidunda.

Nilipoongea na  Kidunda,  aliyetwangana Jumapili na mwanamasumbwi Vasilii Belous pambano la uzito wa kilo 69 – (weltherwight), nilijifunza mengi.
Kwanza nilitegemea Kidunda angekuwa na hasira  au huzuni sana. Wengi tuliotazama pambano la Jumapili tulishtuka namna ambavyo Mtanzania mwenzetu alivyotolewa kwa pointi 20 dhidi ya zake 7.

Jambo la msingi nililoliona kwake Kidunda ni kutotetereka hata kidogo. Alikua mcheshi, katulia kama maji ya mtungi.
Selemani Kidunda   katika kijiji cha Olimpiki London.

“Kushindwa au kushinda ni sehemu ya mchezo wowote ule. Mi bado kijana na bado nina ndoto za kuwa bondia bora Afrika nzima,” ndivyo alivyoanza mazungumzo.

Wakati  tumekaa kijiji cha Olimpiki ilikuja simu toka Radio One, Dar es Salaam na Kidunda akawa anawahakikishia Watanzania kwamba mambo hayajaisha. Na hiyo ilikuwa pia dhana  ya yote aliyonisimulia kwamba safari yake wala haijaisha, ndiyo kama inaanza.

Ni muhimu kuelewa huyu ni “kijana mtulivu sana mwenye nidhamu,” alieleza kocha wake Remmy Ngabo.  Kidunda keshapewa tuzo tatu za Mchezaji Bora wa TASWA (Tuzo inayotolewa  na chama cha waandishi wa Habari Tanzania) mwaka 2010, 2011 na 2012. Huyu  ni bondia aliyeshaiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali za Afrika- Rwanda (2006), Uganda (2011), Msumbiji (2011), Morocco (Aprili 2012) na mara mbili katika michezo ya Jumuiya ya Madola New Delhi , India, mwaka 2010 ambapo alishinda medali ya Shaba. 

Kidunda, basi si mwanandondi aliyeanza shughuli hizi juzi juzi na kubahatika tu kuja Ulaya...
 Mwandishi Freddy Macha nikiwa na Bondia Kidunda,  baada ya mahojiano , kijiji cha Olimpiki London juzi

Ila Olimpiki si mchezo.
Hapa kuna mabondia waliobobea na wengi kutoka Afrika wamekuwa wakitolewa kutokana na kutokua na ufundi au mbinu zinazofikia wenzao wa kimataifa. Mabondia toka Zambia na Gabon, wote wametolewa michuano ya mwanzo. Si Kidunda peke yake.

Kidunda aliyezaliwa Ruvuma mwaka 1984 anasema bondia aliyepambana naye alikuwa na mambo matatu muhimu. 
 
Kwanza “alikuwa na ujanja wa kupiga ngumi mbili tap tap kisha anambana”...ujanja huu unaitwa kwa lugha ya ngumi “clinch” ambao humpa yeye pointi,( ingawa ataonywa na refa) lakini tayari keshaingiza. Ujanja huo Kidunda hakuwahi kuuona. Hivyo imekuwa somo lake. 
 
Kwamba katika ngumi za kimataifa kuna mengi zaidi ya kumpiga mtu. Maana kihistoria Kidunda anasema,  amekuwa akiwatoa wenzake  aliokutana nao nje na ndani ya Bongo kwa pigo kali liitwalo “knockout” si kwa pointi.  

Somo la pili lilikuwa mtindo wa mikono. Vasilii Belous ni mtu anayetumia “south paw” yaani- yeye ni mashoto. Kumpiga mashoto inabidi ugeuke. Akishakupiga anageuka, hivyo unachelewa maana wewe ngumi yako kali ya kuume. Kwa kuwa wewe unamkabili kwa upande wa kulia yeye anafanya ujanja wa kugeuka haraka – hilo ukichanganya na uhuni wa kupiga na kukaba kaba kabali (“clinch”) vyote nilimchanganya kidogo Kidunda. Kocha alivyomshauri aanze kumpiga mwenzie tumboni, sasa mambo yakawa mazuri kwake Kidunda. Lakini muda ulishakuwa umekwenda. Imefikia Raundi ya tatu. 

Alipoanza kumpiga jamaa ngumi za tumbo (mabondia huita “body shots”) akamwona anaanza kusikia kipigo, akaanza kuongeza mambo na ndiyo maana anakiri alipata pointi nyingi zaidi raundi ya mwisho, lakini muda ulishakwisha.  Kifupi ilimchukua muda kidogo kumsoma na kumjua mwenzake, maana yeye kawaida “ ni mwindaji” anayewasoma anaopigana nao kabla ya kuwadunda vizuri. Hana papara.
Selemani Kidunda na kocha wake Remmy Ngabo, wakicheza na sanamu ya sokwe mtu katika bustani za kijiji cha michezo ya Olimpiki, London, juzi Jumatatu.Picha na Freddy Macha

Je,  pambano hili lingekuwa la raundi nyingi zaidi (kama yale mapambano ya kulipwa yenye raundi 10 au 12?).
Selemani: “Ah ningempiga tu.”

Hapo somo jingine. Ikiwa wanamichezo kama Kidunda wangekuwa wanapata fursa kupambana huku nje mara kwa mara wangejua mbinu zaidi.  Lakini si tu kupambana nje. Kwani mbona nchi maskini kama Cuba ina mabondia wazuri vile?
Kocha Ngabo anasema makocha wenzake huku nje  waliwashangaa sana waliposema hawakuwa na michuano mingi  Afrika. Wazungu huwa na michuano mingi, anaeleza Kocha Ngabo na “diary zao zinakuwa zimejaza.Kila tarehe ikipita wanapigana.”

Hilo moja, jingine ni vifaa.
Bondia na kocha wake walilisema sana hili. Kidunda akanitolea mfano wa namna unavyomkuta bondia wa kwetu anatumia begi la uzito usio wake. Kumbe mabegi yana uzito. Kama wewe kilo 56 (“bantam weight”) unatandika begi la uzito wako wakati wa mazoezi. “Matokeo unawakuta mabondia tunajiumiza.”

Mbali na mabegi ni vifaa vya kisasa. Kocha Ngabo na mwanamasumbwi Kidunda wanasimulia namna walivyofurahia vyombo vya mazoezi vilivyowekwa rasmi kwa wanamichezo wa Olimpiki katika chuo cha Bradford kabla ya tukio hili lililoanza Jumamosi tarehe 28.

Kifupi, kuna hilo la kutojionea mengi (“exposure”) yaani elimu dunia. Pili, ukosefu wa vifaa na tatu sisi wenyewe kuwa tunawaunga mkono wanamichezo wetu. Hawa ni watu ambao wanaipenda sana fani yao, na hutumia saa na siku nyingi sana kufanya mazoezi. Bila nidhamu huwezi kufanya kazi ya mtu kama Selemani Kidunda. Tukiwapa pongezi hata pale wanaposhindwa, tukiwaunga mkono wanapokwenda ugenini kwa kuwatungia nyimbo, kuwapigia makofi watapata moyo. Yumkini pia uongozi wetu wa ngazi za chini na juu nao shurti yabidi uangalie suala zima la michezo nchini, kwani si tu ajira bali kitega uchumi.
 
Ikiwa mtoto mdogo au kijana anataka sana kufuata nyayo za bondia mahiri kama Selemani Kidunda atafanyaje?

Maana Kidunda asingekuwa bondia angeishia wapi? Jiulize haya. Kazaliwa kijijini, akamaliza darasa la saba. Leo keshapata tuzo hizo. Kasafiri nchi zote hizo. Hana elimu lakini michezo imejengea nidhamu na uelewa wa ulimwengu. Hilo nalo ni somo muhimu. Kwamba michezo ni ukombozi wa maskini na wanadamu, kiakili, kihisia na kiuchumi.

Tuwaheshimu na kuwapa heko wanamichezo wetu hata pale wanaposhindwa. Jitihada zao ni pia zetu!

Soma zaidi manufaa ya mazoezi na michezo :
www.kitoto.wordpress.com
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!