Sunday, August 5, 2012

"Hii mambo hayeleweki" Aliyepotea miaka minne iliyopita apatikana hai


Kijana Masoud Uliza mkazi wa Mwananyamala Kisiwani aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha miaka minne iliyopita amepatikana akiwa hai baada ya maombi yaliyofanywa na mtume na Nabii Agnes wa Eglaim Ministy kumuibua akiwa hajielewi.

Akitoa ushuhuda wake Jumanne ya wiki hii  katika Kanisa hilo, Uliza alisema tukio hilo lilimtokea katika moja ya Makasino yaliyopo jijini Dar es Salaam, ambapo alikutana na mwanamke majira ya usiku na kukubaliana "wawe pamoja" kwa usiku huo.

Alisema mwanamke huyo alikuwa na gari ambayo haikumbuki namba, na baada ya makubaliano alimuomba waelekee kwanza kwake ndipo wafanye safari nyingine, "Alinichukua hadi karibu na kwake,  nami sikuwa na hofu, nikijiangalia ni kijana tena niliyekabidhiwa mikoba ya uganga na bibi yangu, niliamua kwenda naye kwake ambapo ni karibu na maeneo ya Villa, akaniacha nje. Baada ya hapo sikuweza kujua chochote hadi nilipojikuta baharini nikiwa mtupu” alisema Uliza.

Akasema mwanamke huyo alimtokea na kumwagia maji kichwani, hali iliyomfanya atofautiane na wenzake kwa kila kitu hata kufikia kuwa mzito wa kuongea.

Aliongeza kusema kuwa, kitu cha ajabu anachokikumbuka hadi sasa ni uwezo wa kutembea kwa haraka mithili ya gari kila alipokuwa akitaka kufanya shughuli zake za Uganga.

Kwa upande wake, kiongozi wa Kanisa la Eglaim Ministy, Nabii Agnes akielezea namna walivyomuokoa Uliza alisema, wakiwa katika maombi Kanisani hapo, aliletewa taarifa kuwa kuna mtu hajifahamu na kila wakati anapotea katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema baada ya taarifa hizo, walikwenda kwenye eneo la tukio na kushuhudia na ndipo walizidisha maombi. Kazi hiyo ilikuwa ngumu kutokana na kijana huyo kupotea tena mara kwa mara, “Licha ya utumishi wangu kiukweli niliogopa nikasema itakuweje huyu mtu asiporudi wakati nimeshatoa taarifa polisi kuwa huyu kijana yupo kwangu …hapo ndipo nikazidisha maombi ili Mungu ashushe miujiza yake ya kumkomboa huyu kijana,” alisema Nabii Agnes

Alisema baada ya maombi ya muda mrefu, kijana huyo alifanikiwa kuwa katika hali ya kujitambua na ndipo walipomuuliza, aliwahadithia maisha yake ya nyuma na namna alivyokabidhiwa mikoba yake ya uganga na bibi yake.

Alitoa wito kwa watu kumtegemea Mungu katika maisha yao ya kila siku, kwamba katika Mungu, hakuna kinachoshindikana.

via Habari Mseto blog
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!