Thursday, August 2, 2012

Mbunge ahusishwa na waliokamatwa wakisafirisha bangi kwenda ng'ambo

MBUNGE wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokea mkoani Tabora, anahusishwa na wanawake waliokamatwa wakisafirisha bangi kwenda nje ya nchi, Raia Mwema limefahamishwa.

Raia Mwema limejulishwa kwamba mmoja wa watuhumiwa waliokamatwa na bangi na kufikishwa mahakamani, Hadija Magesa ni ndugu wa mbunge huyo na jina lake halisi ni Hadija Tambwe Abdallah, na kwamba walikuwa pamoja muda mchache kabla ya wote kuanza safari kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Taarifa zilizopatikana zinaonyesha kwamba *Mbunge huyo aliondoka nchini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates namba EK 726, Julai 28, 2012 kwenda Italia, saa chache kabla ya Hadija na mwenzake, Sasha Mnyeke, kukamatwa wakitaka kuondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki TK 604 Julai 29, 2012 kwenda  Instabul, Uturuki.

Uchunguzi wa Raia Mwema umethibitisha kwamba *Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wabunge waliomo ndani ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayotuhumiwa kwa rushwa, aliaga bungeni kuwa anasafiri kwenda nchini India, kumpeleka mama yake mzazi kwa matibabu.

Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel amesema mjini Dodoma kwamba *Mbunge huyo ana ruhusa ya shughul binafsi kwenda nje ya nchi.

“Amekwenda India kumpeleka mama yake mzazi kwenye matibabu,” amesema Joel.

Tayari Khadija na Sasha wamekwishakufikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na biashara hiyo wakati *Mbunge huyo akiwa nchini Italia akitarajiwa kurejea nchini Agosti 2, mwaka huu kupitia Dubai.

Katika mazingira tata Hadija anamiliki hati ya kusafiri AB 151604 ikiwa na jina la Hadija Magesa wakati tiketi yake ikiwa na jina la Hadija Tambwe, jambo ambalo limeelezwa kuibua utata uliosababisha kukamatwa kwao kabla ya kuondoka Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Raia Mwema unabainisha ya kuwa Julai mosi mwaka huu *Mbunge huyo alipata kusafiri nje ya nchi na kurudi akitokea Dar es Salaam kwa njia hiyo hiyo aliyosafiri Julai 28, 2012 kwa ndege ya Emirates EK 726.

Juhudi za kuwasiliana na *Mbunge huyo huko aliko azungumzie tuhuma zinazoelekezwa kwake hazikuzaa matunda.

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, ameliambiaRaia Mwema kwamba makachero wanaendelea na uchunguzi kujua mtandao mpya wa dawa za kulevya unaohusisha watu maarufu kutokana na taarifa wanazopokea.

Raia Mwema  inazo taarifa za ndani ya kuwapo kwa mtandao wa wafanyabiashara wanaotumia baadhi ya wanawake kusafirisha ya dawa za kulevya kwenda nje ya nchi, baadhi wakiwa watu wenye mahusiano ya kidugu.

Kuhusishwa kwa *Mbunge huyo katika taarifa hizi za bangi kunachangia katika wiki  ambayo inaweza kutajwa kuwa ni mbaya sana kwa *Mbunge huyo wa Viti Maalumu ambaye amekuwa akitajwa sana katika sakata lililoibuka bungeni wiki iliyopita likiwawatuhumu baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kwa kufisadi Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Kamati hiyo sasa imevunjwa na Spika Anne Makinda kutokana na hoja iliyowasilishwa na *Mbunge wa Namtumbo, Vita Rashidi Kawawa, akiomba kamati hiyo ivunjwe kwa kulidhalilisha Bunge, pamoja nayo na kamati nyingine zenye kuelekezewa tuhuma za ufisadi.

Kati ya tuhuma zinazoelekezwa kwa *Mbunge huyo, ambazo kwa pamoja na nyingine zitachunguzwa na Bunge lenyewe ni kampuni yake kufanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO.

---
* Jina la Mbunge huyo limetajwa kwenye gazeti la RaiaMwema ilikonukuliwa hapa.
RaiaMwema.co.tz
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!