Wednesday, August 1, 2012

Msabaha (Mb) apendekeza wenye VVU/UKIMWI wabainishwe jamii iwajue; Dkt. Kigwangalla asema si wazee wote wastahili tiba bure, wengine (mf. Sitta, Lowassa) mbona wanajiweza?


MBUNGE wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (CHADEMA) ameitaka Serikali kutafuta njia itakayowasaidia wananchi ili wawatambue watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na wasioishi na virusi hivyo.

Msabaha alitoa kauli hiyo bungeni jana, wakati akitoa maoni yake kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iliyowasilishwa juzi na kujadiliwa kwa siku mbili.

Katika maoni hayo, mbunge huyo alisema dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) zimekuwa zikisababisha watu wanenepe kupita kiasi na wengine kujikuta wakizidisha matamanio.

Kutokana na kuzidisha matamanio huko, Msabaha alisema kumesababisha wananchi wasijue nani anaishi na virusi hivyo na nani hana huku kukitoa fursa kwa wengine kuambukiza wenzao kwa makusudi.

Mbunge huyo wa CHADEMA kutoka Zanzibar, mbali na kauli yake hiyo ambayo ni wazi itasababisha mgogoro na wanaharakati wa masuala ya jamii kwa kuwa inaashiria unyanyapaaji, alikwenda mbali zaidi na kusema bora fedha za kupambana na Ukimwi ambazo zimelalamikiwa kuwa kidogo, zisiongezwe.

Kauli hiyo ya kutoongezwa kwa fedha hizo, ilipingana na maoni ya wabunge wengi ambao walitaka bajeti ya wizara hiyo, iongezwe huku wakitaka kuwapo kwa mfuko maalumu wa fedha za UKIMWI na kuepuka kutumia fedha nyingi za misaada.

Wakati Msabaha akipendekeza hilo, Mbunge wa Viti Maalumu, Zarina Madabida (CCM), alitaka wagonjwa wengine wakiwamo wa Ukimwi wenye uwezo wasipewe ARV bure, badala yake watozwe fedha ili zitumike kwa wagonjwa wengine ambao hawana uwezo, “Yaani tunatoa ruzuku kwa watu wote? Mbunge naye anapewa dawa mseto kwa bei ya ruzuku ya Sh 1,000 badala ya Sh 4,500, kwa nini? Hata katika UKIMWI nako wenye uwezo wanunue ARV ili Serikali itumie ruzuku kwa watu wenye uhitaji,” alisema Madabida.

Naye Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla (CCM), alipendekeza Serikali isitoe matibabu bure kwa kila mzee pamoja na kuwa ipo sera ya matibabu bure kwa wazee walio na umri wa kuanzia miaka 60, “Wale wenye uchumi mkubwa wakamuliwe na Serikali, ili kinachopatikana kikawasaidie wenye uchumi mdogo… watu wako tayari kuchangia afya, kwa nini wapewe huduma bure? Mtu kama Sitta (Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel) na Lowassa (aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward) ni wazee, kwa nini watibiwe bure?” alihoji.

Naye Mbunge Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alitaka Serikali kuingia mkataba na madaktari bingwa inayowafundisha, ili wakitaka kuondoka nchini, iwabane. Alisema kusomesha daktari bingwa inachukua miaka 12, lakini anaachiwa kuwa na uhuru wa kuondoka kwenda kufanya kazi popote na kuhoji gharama za Watanzania wanafidia kina nani?

via HabariLeo
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!