Wednesday, August 1, 2012

Mtanzania mwingine ayaaga mashindano ya Olimpiki London 2012

Picture: Tanzania team to the London 2012 Olympics Ammaar Ghadiyali na Magdalena Moshi
Mtanzania Ammaar Ghadiyali amefuata nyayo za bondia Seleman Kidunda kuaga mapema Michezo ya Olimpiki 2012 baada ya kutolewa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kuogelea ya mita 100 ‘freestyle’ yaliyofanyika jijini London, Uingereza jana.

Ammar ambaye, hata hivyo, ushiriki wake ulikuwa ni wa kujifurahisha kwavile hakufuzu na alicheza Olimpiki kupitia nafasi maalum za upendeleo,alishindwa vibaya jana baada ya kushika nafasi ya 57 kati ya washiriki 62 akitumia muda wa dakika 1:05.

Ammaar Ghadiyali, aliyeshika Bendera ya Taifa, aaga mashindano ya Olimpiki 2012

Mashindano hayo ya awali ya wanaume yalikuwa ni ya kusaka washindi 16-Bora ambao wamesonga mbele katika safari yao ya kuwania medali.

Mwakilishi mwingine wa Tanzania, Magdalena Moshi, ambaye pia hakufuzu kama Ghadiyali, anatarajia kujifurahisha leo katika mashindano ya kuogelea ya mita 100 (wanawake).

Magdalena, kama ilivyokuwa kwa Ghadiyali, hatapewa medali hata akishinda kwa sababu hakufuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2012 na atashiriki kupitia nafasi maalum za upendeleo zinazotolewa na shirikisho la mchezo huo duniani (FINA) kwa nchi ambazo zimeshindwa kabisa kuwa na muogeleaji hata mmoja aliyefuzu.

Baada ya bondia Kidunda kudundwa kirahisi kwa pointi 20-7 dhidi ya bondia Vasilii Belous wa Moldova katika pambano la hatua ya awali lililofanyika juzi la kusaka washindi 16-Bora, matumaini ya Tanzania sasa yamebaki kwa wanariadha wanne tu ambapo mwanadada Zakia Mrisho atachuana Agosti 8 katika mbio za mita 5,000.

Wanariadha wengine wa mbio za Marathon, Samson Ramadhan, Mohamed Msenduki, na Faustine Mussa watatupa karata zao Agosti 12.

---
Israel Saria,
TanzaniaSports.com
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!