Friday, August 3, 2012

Sitta: Tuko tayari kwa chokochoko za Malawi

Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni, Samuel Sitta,
Uhusiano kati ya Tanzania na Malawi upo hatarini baada ya serikali ya Malawi kutangaza kwamba ziwa Nyasa ni mali ya Malawi kwa asilimia 100 ilhali sehemu ya ziwa ipo Tanzania.

Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Godfrey Zambi, aliliambia Bunge jana alipoomba mwongozo wa Spika akieleza kuwa vyombo vya habari vya Malawi na vya Tanzania vimemkariri mmoja wa makatibu wakuu wa Malawi, akieleza kwamba ziwa Nyasa lipo nchi mwake kwa asilimia mia, hali ambayo inahatarisha uhusiano wa nchi hizo.

“Ni vyema serikali ikatoa maelezo juu ya hali ya ziwa Nyasa ili wananchi wa Mbeya na wabunge hapa tuelewe, maana kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mpaka wa ziwa hili na hatujui kilichofikiwa,” alisema.


Alisema taarifa za katibu huyo zinatia wasiwasi na hofu kwa wananchi wa Mbeya ambao wanatumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema suala hilo atalipeleka serikalini ili Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alitolee ufafanuzi na taarifa kamili.

Hata hivyo, Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni, Samuel Sitta, alisema serikali imestushwa sana na taarifa hizo kwa kuwa mazungumzo kuhusu mpaka wa ziwa Nyasa yanaendelea.

Alionya kwamba Tanzania ipo tayari kwa uchokozi wowote kwa kuwa inafuata sheria za kimataifa, hivyo akawataka wananchi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, ambayo inapakana na ziwa hilo kuendelea na shughuli zao za kiuchumi ziwani humo.

Alisema kauli rasmi ya serikali kuhusu jambo hilo itatolewa bungeni Jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wakati huo huo, ratiba mpya ya Bunge inaonyesha kwamba Mkutano wa Nane unaoendelea sasa utamalizika Agosti 16 badala ya 22 iliyokuwa imepangwa awali ili kutoa fursa kwa wabunge Waislamu kwenda kusherekea sikukuu ya Idd na familia zao.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!