Thursday, August 16, 2012

"NAWASHANGAA WANAONIFIKIRIA KUWA BADO NI TEJA"....LANGA

Katika vijana wenye mfano halisi wa jinsi madawa ya kulevya yanavyoweza kuharibu maisha ya mtu, Langa ni wa kwanza .

Amewahi kuwa teja aliyekubuhu kiasi cha kumharibia mambo mengi na heshima kwa watu wanaomfahamu.


Hata hivyo kwakuwa ameshaacha na kuamua kuwa kijana mwema, anakerwa na jinsi baadhi ya watu wanavyoendelea kumchukulia bado ni teja.


Akiongea na kipindi cha Power Jams cha East Africa Radio jana, Langa amesema tabia hiyo imemfanya aanze kufikiria kubadilisha kazi ili watu wamsahau kabisa.


Alisema fikra hizo zinamkatisha tamaa na haelewi kwanini watu hawawezi kuamini kuwa binadamu anaweza kubadilika.


“Inauma sana kama utasingiziwa kuwa unafanya kitu ambacho wewe hufanyi, jambo hili linalonifanya nifikirie kubadilisha kazi na harakati nazofanya ili wanisahau kabisa,” alisema.


Langa aliwahi kuongea mambo mengi kuhusu maisha ya uteja kwenye kipindi cha FidStyle Friday cha July 8 mwaka jana.


“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha katika hali hiyo ni dawa za kulevya. Kwa miaka mitano nilitumia sana Cocaine, Heroin, bangi na pombe. 


Namshukuru Mungu sasa nimerejea katika hali yangu.Siamini kama nimenusurika kwa sababu madawa yalinitesa, nikafanya mengi ya ajabu yaliyoichukiza familia yangu na marafiki ikiwa ni  pamoja na kuwa mwizi na mkabaji mitaani na nyakati za usiku,” alisema Langa ambaye kundi lao la Wakilisha lilitamba na nyimbo kama `Unaniacha Hoi’ na `Kiswanglish’.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!