Thursday, August 9, 2012

WASHINDI WA MBIO ZA BAISKELI MKOANI SHINYANGA WAKABIDHIWA ZAWADI ZAO

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Wilson Nkhambaku(kushoto) akimkabidhi Seni Konda kitita cha shilingi milioni moja ikiwa ni zawadi baada ya kuibuka mshindi katika mashinmdano ya Baiskeli Kanda ya Ziwa yaliyozaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia kinywaji chake cha Safari Lager wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku Kuu ya Wakulima ya Nane nane.Kulia ni Ofisa mauzo wa Kanda ya Ziwa, Malaki Sitaki.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Wilson Nkhambaku(kushoto) akimkabidhi Elizabeth Clement kitita cha shilingi laki saba ikiwa ni zawadi baada ya kuibuka mshindi katika mashinmdano ya Baiskeli Kanda ya Ziwa yaliyozaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia kinywaji chake cha Safari Lager wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku Kuu ya Wakulima ya Nane nane.Kulia ni Ofisa mauzo wa Kanda ya Ziwa, Malaki Sitaki.
Washiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli wakishindana wakati wakimaliza mbio hizo katika uwanja wa mpira wa Kambarage mjini Shinyanga.
Mmoja ya washiriki wa mashindano ya mbio za baiskeli wanawake akimalizia mbio za kilometa 150.
Baadhi ya Baiskeli za wakazi wa Kanda ya ziwa wakiwa wamezipaki mara baada ya mashindano hayo wakimsikiliza mgeni rasmi

MKAZI wa Manispaa ya Shinyanga Seni Konda, ameibuka bingwa upande wa Wanaumena na kuzawadiwa kitita cha Shilingi Milioni moja katika mashindano ya Mbio za Baiskeli Kanda ya Ziwa za Kilometa 220 kutoka Shinyanga mpaka Wilayani Kahama na kurudi Shinyanga zilizofanyika Mkoani Shinyanga wakati wa kusherehekea Siku Kuu ya Wakulima ya Nanenane kwa udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania kupitia Bia yake ya Safari Lager.

Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha washiriki zaidi ya 200 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi mshindi wa pili alikuwa ni Leonard Ng’wigulu pia kutoka manispaa ambaye pia alijinyakulia zawadi ya shilingi 800,000 ambapo mshindi wa tatu Charles Makhirikhiri kutoka Shinyanga vijijini alijinyakulia kitita sha shilingi 600,000.

Mshindi wanne Charles clement alipata zawadi ya shilingi 500,000 ambapo wa tano Nyanda Duba alijinyakulia shilingi 300,000 na mshindi wa sita hadi wa kumi walipatiwa kifuta jasho cha shilingi 100,000 kila mmoja.

Kwa upande wa washiriki wanawake waliokimbia umbali wa kilometa 150 kutoka Shinyanga mjini hadi Isaka na kurejea tena Shinyanga mjini, Elizabeth Clement aliibuka mshindi wa kwanza na kupata zawadi ya shilingi 700,000 ambapo mshindi wa pili Salome Donald alipata shilingi 500,000 na mshindi wa tatu Berth Donald alijinyakulia shilingi 300,000.

Mshindi wa nne kwa upande wa wanawake alikuwa ni Nyazobe Masanja aliyepata shilingi 200,000 na mshindi wa tano Rabi Ng’wandu aliyejinyakulia shilingi 150,000 ambapo pia kwa mshindi wa sita hadi wa kumi kila mmoja alijipatia shilingi 100,000 kama kifuta jasho.

Mashindano hayo pia yalihusisha mbio za walemavu waliotumia baiskeli za matairi matatu ambapo walizunguka uwanja wa mpira wa Kambarage mizunguko 30 ambapo alikuwa ni Makande Ndelela kutoka manispaa aliyepata shilingi 100,000, mshindi wa pili Petro Thomas, shilingi 80,000 na watatu Ngalu Ngamba aliyejinyakulia shilingi 60,000.

Akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo ambazo zimedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, mgeni rasmi Wilson Nkhambaku ambaye ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga aliwapongeza washiriki wote walioshiriki katika mashindano hayo.

Nkhambaku alisema michezo ni moja ya sera za chama tawala CCM, lakini pia mbali ya kuwa ni burudani lakini hutoa ajira kwa vijana wanaoshiriki michezo hiyo.

Aidha aliipongeza kampuni ya bia (TBL) ambapo aliwataka kuendelea na moyo huo na kuiomba kufikiria uwezekano wa kuongeza viwango vya zawadi kwa washiriki na kwamba ni vizuri mwakani kampuni ikatoa zawadi kwa washiriki wote watakaojitokeza kushiriki mashindano hayo kwa viwango tofauti ili mradi kila mshiriki aweze kujipatia chochote na kwamba kitendo hicho kitawapa moyo wa kushiriki vijana wengi.

“Nakupongezeni sana kwa moyo wenu wa kuwadhamini mashindano haya ya mbio za baiskeli ikiwa leo hii ni mwaka wenu wa 15, hongereni sana, lakini niwaombe kitu kimoja ni vizuri sasa mwakani mkaangalia uwezekano wa kuongeza viwango vya zawadi ili iwe kivutio cha washiriki wengi kushiriki,” alisema Nkhambaku.

Kwa upande meneja mauzo kanda ya Ziwa wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Malaki Staki alisema kampuni yake imekuwa ikidhamini mashindano ya mbio za baiskeli kwa mikoa ya kanda ya ziwa kwa lengo kukuza mchezo huo ambao unapendwa na wakazi wengi wa mikoa ya kanda ya ziwa.

Staki alisema mbali ya kukuza mchezo huo wa mbio za baiskeli lakini pia umelenga kuwapatia kipato vijana wa kike na wa kiume wanaojitokeza kushiriki mashindano hayo.

“Kwa mwaka huu kampuni yetu imetumia kiasi cha shilingi milioni 5.9 kwa ajili ya zawadi mbalimbali kwa washiriki tofauti na mwaka jana ambapo tulitumia shilingi milioni 2.5, lakini pia mchezo huu ni moja ya burudani kubwa kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa, ambao sasa tunawaomba waendelee kutumia bia yetu ya safari kwa wingi ili tuendelee kudhamini mchezo huu,” alisema.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!