Sunday, October 21, 2012

JWTZ WAMTANDIKA VIBAO TRAFIKI KISA KIKIWA NI KUWACHELEWA KATIKA FOLENI


ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , jana walimshambulia kwa kumpiga, Askari wa Kikosi cha Usalama  Barabani katika makutano ya Barabara za Morogoro, Mandela  na Sam Nujoma, Ubungo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Chares Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa wahusika walikuwa wakihojiwa katika Kituo cha polisi Buguruni na uchunguzi unaendelea.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa tukio hilo lililokuwa kama sinema, lilidumu kwa takriban dakika 15 lilimkumba trafiki aliyetajwa kwa jina la Mpemba, ambaye alikuwa akitimiza wajibu wake wa kazi kwa kuongoza magari eneo hilo.

Walieleza kuwa wakati Mpemba akiendelea na kazi hiyo alivamiwa na askari wa JWTZ wanaokadiriwa kuwa 15 waliokuwa  kwenye msafara wakitokea eneo la Mwenge, kupitia Barabara ya Sam Nujoma walidai kuwa trafiki huyo aliwarushia matusi ya nguoni.

Wakati trafiki huyo akiamuru magari yaliyokuwa yakitokea eneo la Mwenge kusimama ili kuruhusu magari ya upande mwingine kupita, gari la jeshi lilikuwa lipo mbele kusubiri zamu yake kuruhusiwa, lakini ghafla dereva wa gari hilo aliamua kupita bila kufuata maelekezo ya trafiki jambo linalodaiwa kuwa lilimkasirisha Mpemba na kuwatolea JWTZ maneno ya kuudhi.

“ Huyu trafiki alipoona wale JWTZ  wamekatiza kwa ghafla wakati yeye alikuwa akijiandaa kuita magari ya upande mwingine, aliwatolea maneno fulani, ndipo ghafla tukaona wamesimamisha gari lao katikati ya barabara na mwanajeshi mmoja akashuka kwenye gari na kumzonga trafiki,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyeomba kutokuandikwa jina kwa sababu za kiusalama.

Shuhuda mwingine alisema: “Baada ya kuona yule mwanajeshi ameshuka ndani ya gari, trafiki mmoja aliyekuwa pembeni akasogea kwa hasira akihoji sababu za mwenzake kufanyiwa vile. Mara akatokea mwanajeshi mwingine kwenye gari lao na kumvua kofia yule trafiki mwenye hasira.”

Alisema kuwa kitendo cha trafiki huyo kuvuliwa kofia yake kiliamsha hasira zaidi na kumfanya achukue uamuzi wa kumrushia ngumi askari wa JWTZ, ndipo kundi la wanajeshi wengine walimkaribia trafiki huyo na kuanza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili. 

Shuhuda mwingine alisema kuwa trafiki mwingine aliyekuwa akishuhudia tukio hilo akiwa kando ya barabara alifanya jitihada za kuwasiliana na wenzake kwa njia ya redio maalumu (radio call) ambaoo walifika katika eneo la tukio na kumpeleka Mpemba hospitalini kwa matibabu huku wanajeshi hao wakiendelea na safari yao wakiwa kwenye malori matatu. 

Hata hivyo, habari zinasema kuwa kutokana na  mawasiliano ya polisi wanajeshi hao hawakufanikiwa kufika mbali na kabla ya kuvuka eneo la Buguruni Mataa walikamatwa.

Kauli ya polisi
Kamanda Kenyela alisema: “Hata hawakufika mbali, mawasiliano yamefanyika mapema na tukafanikiwa kuwakamata. Hata hivyo  idadi yao bado sijaijua. Hili ni  tukio la kufanyia uchunguzi ila taarifa za awali ndiyo hizo.

 Taarifa zingine nategemea kuzipata kesho, kwa hiyo ukiniuliza nitakuwa na taarifa zote.”

Hii si mara ya kwanza kwa askari wa JWTZ kuwapiga trafiki wakiwa kazini, ambapo mara kadhaa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange ameonya kuwa askari yeyote wa jeshi hilo atakayethibitika kuhusika na matukio kama hayo atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!