Tuesday, December 18, 2012

LULU MICHAEL ASHITAKIWA KWA KOSA LA KUUA BILA KUKUSUDIA.......KESI ITAANZA KUSIKILIZWA DISEMBA 21MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, aliyekuwa anakabiliwa na mashitaka ya kumuua msanii mwenzake Steven Kanumba kwa kukusudia, amebadilishiwa hati ya mashitaka na sasa anashitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia.


Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.

Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga alidai kuwa upelelezi umekamilika ambapo mahakama imepanga Desemba 21, mwaka huu kumsomea Lulu maelezo ya kesi pamoja na ushahidi ambao upande wa mashitaka utautumia katika kesi hiyo.

Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika hatua ya upelelezi na sasa itahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ambapo mshitakiwa ataruhusiwa kujibu mashitaka dhidi yake.

Kwa mujibu wa sheria, kutokana na Lulu kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata dhamana.

Lulu aliposikia kuwa upelelezi wa kesi yake umekamilika alifurahi na kuanza kucheza kwenye kiti na alipotoka katika chumba cha mahakama, aliendelea kucheza huku akirukaruka.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani Steven Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua msanii huyo nyota wa filamu nchini.
Hata hivyo, kabla kesi haijaanza kusikilizwa, tayari ilishafika Mahakama ya Rufani, baada ya kuibuka kwa utata wa umri wa mshitakiwa huyo.

Utata huo uliibuka baada ya mawakili wanaomtetea msanii huyo, kuomba kesi hiyo isikilizwe katika Mahakama ya Watoto kwa madai kuwa Lulu bado mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyoonesha katika hati ya mashitaka.

Mahakama Kuu ilikubali kuchunguzwa kwa umri wa Lulu, lakini Mahakama ya Rufani ilitengua uamuzi huo na kuamuru kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama ya Kisutu kuendelea.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!