Saturday, December 22, 2012

LULU MICHAEL ASOMEWA MAELEZO YA AWALI YA KESI YA KUUA BILA KUKUSUDIAUPANDE wa mashitaka katika kesi inayomkabili msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, jana ulimsomea maelezo ya awali ya kesi inayomkabili na ushahidi watakaoutumia pale kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro, alisema kesi hiyo itakapoanza upande wa mashitaka utaleta mashahidi tisa na kwamba ushahidi wa nyaraka pia utawasilishwa.

Mashahidi watakaotoa ushahidi wao Mahakama Kuu ni pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, Sofia Kassim, Daktari wa marehemu aitwaye Pancras Kageigwa, Morris Semkwao na Esther Zephania ambaye ni askari Polisi wa kituo cha Oysterbay, Kinondoni.

Mashahidi wengine ni Daniel Shila, Margaret Kibobo na askari mwenye namba E5056, Sajenti Elinatus.

Alisema pamoja na ushahidi wa nyaraka, kutakuwa na ripoti ya uchunguzi wa hospitali na ramani ya eneo la tukio. 

Hakimu Augustina Mmbando ambaye kesi hiyo ilifika kwake kwa hatua za awali alisema Lulu hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Mshitakiwa huyo ambaye amebadilishiwa shitaka kutoka mauaji hadi kuua bila kukusudia, alirudishwa tena rumande mpaka kesi hiyo itakapopangiwa tarehe nyingine.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwa Steven Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua bila kukusudia msanii huyo nyota wa filamu nchini.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!