Saturday, December 22, 2012

SERIKALI YABEBA JUKUMU LA KUMSAIDIA SAJUKI HADI KUPONA


Serikali imechukua jukumu la kumhudumia msanii na muongozaji wa filamu Sadick Juma Kilowolo ambaye anatarajia kuondoka wiki ijayo kuelekea India kwa matibabu.

Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Wilson Makubi, alisema Sajuki ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, amegundulika kuwa ana tatizo la kufeli kwa figo na kwamba yuko chini ya uangalizi na uchunguzi zaidi.

Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imejitolea kumsafirisha msanii huyo kwa gharama zake na kusaidia katika gharama za matibabu akiwa nchini India.

“Sajuki anatarajiwa kusafiri wiki ijayo baada ya taratibu zote kukamilika, hivyo sisi kama TAFF tunathibitisha kuwa hali yake bado haijatengemaa kama ilivyojulikana hapo awali,” alisema Makubi.

Msanii huyo amekuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu ambapo mwaka jana alianza na uvimbe ulioanzia mikononi na baadaye ndani ya mwili kwenye ini na sehemu tofauti za tumbo.

Msanii huyo alipelekwa India kwa ajili ya kutibiwa, kisha akarejea nchini baada ya kupata nafuu, ambapo kwa sasa ameugua tena na anahitaji matibabu ya haraka ikiwamo upasuaji.

==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!