Saturday, May 28, 2016

Wabunge walia na mifumo ya elimu kubadilikabadilika


WABUNGE bila kujali tofauti zao za kiitikadi, wamelalamikia mitaala mibovu inayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ikiwemo kila waziri kufika na mfumo wake. Pia wamelalamikia mitaala kukosewa na kutaka Rais John Magufuli kuifumua wizara hiyo na kuiunda upya.

Wakichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo juzi jioni bungeni, wabunge hao walionesha kukerwa na jinsi wizara isivyo na mtaala wa aina moja. Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema Waziri akiingia katika wizara ndiyo mfumo, huku akimtaja Waziri aliyepita, Dk Shukuru Kawamba, kwamba aliyoyafanya yamepinduliwa yote na Waziri Ndalichako ambaye alidai akiondoka, atakayekuja atayapindua yote.

“Hii inatia tatizo sana, hivi mambo ya BRN (matokeo makubwa sasa ) yameenda wapi?” Alihoji? Alisema Sera ya Vitabu ya Mwaka 1991, iliruhusu sekta binafsi waandike vitabu na taasisi ya elimu wakague vitabu na kuhoji ni nani anahariri vitabu leo hii, huku akidai kuwa magazeti yanahaririwa vizuri siku hizi kuliko vitabu vya shule.

Mbatia alisema Sera ya Elimu iliyozinduliwa mwaka jana imetumia zaidi ya Sh bilioni 50, lakini katika ukurasa wa 22 inaelezwa kuwa mtaala unafundishwa, huku ukurasa wa 27 ukisema mtaala ni mwongozo mpana. Alisema kuna kitabu kimeandikwa mbili mara saba kinasema 15, kitabu cha hisabati darasa la kwanza pale mwanzoni kinasema namba nzima ni 1 hadi 99, ukiangalia cha Kiingereza Chapter 4 inaanza na aeiou wakati mwanzoni ndiyo wanaanza na sentensi ni vitu vya ajabu sana.

“Elimu ndiyo mapigo ya moyo ya taifa, mapigo hayo ya moyo yakizimika taifa nalo limezimika. Hivyo namwomba Rais Magufuli afumue wizara yote ya elimu kwani kuna ufisadi wa kutisha hasa taasisi ya elimu ndiyo hovyo kabisa,” alisisitiza. Mbunge wa Mwibala, Kangi Lugola (CCM) alisema kila waziri anakuja na mfumo wake kwa kuanzisha mitaala yake kwa kufumua ya mwenzake aliyetangulia.

“Waziri lazima hili kuliangalia haiwezekani kila waziri anayekuja kuwa na mfumo wake kwa kufumua ya wengine, jambo linalofanya kusiwe na mfumo mmoja wa mtaala,”alisema. Naye mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Hassan (CHADEMA) alisema mitaala iliyopo sasa haiendani na soko la ajira nchini na hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na inawaacha watoto masikini katika ombwe kubwa.

Naye Mbunge wa Maswa, Mashimba Ndaki (CCM) alisema baada ya kuweza elimu bure, kulikuwa na suala la kujenga maabara ambalo limetoweka na kuanza ununuzi wa madawati. Huku akishangaa suala la ununuzi wa madawati yanakaa wapi wakati shule nyingi hazina majengo ya kutosha. Naye,Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mahawe (CCM) alisema kwa sasa nchini hakuna mfumo maalum wa mitaala ya kufundishia kutokana na kubadilishwa kila wakati bila kuwa na tija.

Alisema hatua hiyo inatokana na kila waziri kuja na masuala yake kwani zamani kulikuwa ma mfumo mmoja nchi nzima, hivyo ni vema kuangaliwa ni wapi wizara hiyo ilianguka na kusimama kisha kuendelea kuboresha elimu.

“Nakumbuka miaka ya nyuma kulikuwa na mashairi tunaimba wanafunzi wa nchi nzima kama ile ya ‘Karudi baba mmoja toka safari ya mbali kavimba miguu,kutokana na kuwa na mtaala mmoja,’” alisema.

Naye Mbunge wa Bihalamulo Magharibi (CCM), Oscar Mukasa alisema suala la mitaala limekuwa tatizo nchini hasa baada ya walibadilisha mitaala hivi karibuni ya darasa la kwanza na la pili na kuleta KKK yaani kuandika, kuhesabu na kusoma na sasa walimu wanabahatisha tu. Alisema hatua hiyo inatokana na kuwa awali walikuwa na mtaala mwingine ambao kabla haujaonesha mafanikio yeyote umeondolewa hivyo wanafunzi wanabaki wakibabaika.

Mbunge huyo alikuwa na vitabu vitatu vya Sayansi viwili vya darasa la sita na kimoja darasa la saba, lakini kila kimoja kikieleza aina za ubongo tofauti. Alisema kimoja cha darasa la sita kinaeleza ubongo una sehemu tatu na kile cha darasa la saba ubongo una sehemu nne na kutaka vitengo vya ukaguzi kuimarishwa ili kujua wanafunzi wanafundishwa nini.
Mbunge Asunga, alisema ni vema wizara hiyo kuangalia mitaala kwani ya sasa haiwafanyi vijana kujitegemea kwa kutoendana na vipaumbele vya nchi kuendana na soko la ajira. Naye, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Maftah Nachuma (CUF) alisema suala la elimu limekuwa likiwekwa danadana kwa kila waziri anayeingia na kuja na mitaala yake kwa kubadilisha mfumo wa elimu.

“Kila waziri anayekuja na kutunga sera za elimu mwisho wa siku,taifa hatuna sera wala mitaala mmoja tunabaki tunayumba yumba na hatuwezi kufikia malengo ya Mwalimu Nyerere kuweza kujikomboa mwenyewe wala jamii inayomzunguka,” alisema.

Alisema hawezi kujikomboa kwa kuwa elimu anayopata kwa kuwa haina dira wala muelekeo inakuwa si elimu bora, kwa kuwa kuna wizara mbili ya Tamisemi na Elimu zinashughulikia elimu. Alisema yeye akiwa mkuu wa shule kwa miaka 12 hajui tofauti ya vitu vinavyoshughulikiwa na Wizara ya Tamisemi na Wizara ya Elimu na kuona kitu kimoja.

Naye Mbunge wa Mbozi, Pascal Ahonga (CHADEMA) alisema suala la mitaala kila mtu anapanga ya kwake kila waziri anachanganya kutokana na ukosefu wa viongozi bora.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!