Saturday, May 28, 2016

Walioharibu uchaguzi Zanzibar wachunguzwa

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema uchunguzi unaendelea kuwabaini watu waliohusika na kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25 na kusababisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuitisha uchaguzi mwingine wa marudio.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Fuoni, Yussuf Hassan Iddi aliyetaka kufahamu waliovuruga uchaguzi wa Oktoba 25 wamechukuliwa hatua gani hadi sasa.

Alisema uchunguzi wa kina unahitajika kwa sasa ikiwemo kukusanya vielelezo kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwemo watendaji wa Tume ya uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi ambao waliohusika na matukio hayo.

Alikiri na kusema suala hilo limechukua muda mrefu takriban miezi saba tangu uchaguzi huo kufutwa na kufafanua kuwa kufungua mashtaka kunahitajika uchunguzi wa kina. “Mheshimiwa Spika napenda kusema kwamba Serikali ipo katika hatua za uchunguzi wa tukio hilo ambalo linahitaji muda mrefu wa kufuatilia wale wote waliohusika,” alisema.

Aboud alisema mara baada ya uchaguzi wa Oktoba kuvurugika, serikali ilifanya wajibu wake kwa kuipatia fedha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kuiwezesha kufanya uchaguzi mwingine.

Alisema uchaguzi wa marudio ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu na viongozi kuchaguliwa na kushika hatamu ya kuongoza nchi.Aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa serikali haijalifumbia macho suala hilo kwa sababu imetumia fedha nyingi za dharura kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi wa marudio unafanyika.

“Serikali kamwe haijalifumbia macho suala la watendaji waliovuruga uchaguzi wa marudio na kupelekea kuitia hasara serikali...suala hilo lipo katika mikono ya vyombo vya uchunguzi na upelelezi kwa hatua nyingine,” alisema.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kwa madai ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali ambazo zilionesha kwamba uchaguzi huo usingekuwa huru na haki na kuibua malalamiko pande zote.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!