Saturday, May 21, 2016

WANAOBADILISHA TAKA KUWA BIDHAA WAOMBA KUTAMBULIWA

Balozi wa kujitolea wa mazingira, Omary Kombe ameiomba Serikali kuwatambua watu wanaobadilisha taka kuwa bidhaa kwa kuendeleza taaluma hiyo ili kuinua uchumi na kuondokana na tatizo la uchafu nchini.

Akiongea na waandishi wa habari  Mei 18, 2016 jijini Dar es Salaam, Kombe  alisema kwamba kwa kuwatambua watu hao, tatizo la taka litakwisha kwa kiwango kikubwa nchini hasa katika jiji la Dar es Salaam.

“Wapo watu ambao mara nyingi tunawaona kwenye maonyesho mbalimbali kama vile sabasaba ambao wanauwezo wa kubadili taka kuwa bidhaa za majumbani kwa mfano, mkaa, mapambo na bidhaa nyingine, ni vizuri Serikali ikawatumia  watu hao kuondokana na tatizo la taka nchini,” alisema Kombe.

Aliongeza kwamba, mazingira bado ni machafu licha ya serikali ya awamu ya tano kuweka  mkazo katika suala zima la usafi kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Kombe alisema kwamba, tatizo hilo la uchafu litatatuliwa kama watu wenye uwezo wa kubadilisha taka kuwa bidhaa watatambuliwa na kufanya kazi hiyo kuwa rasmi.

Aidha alisema kuwa, kwa kubadilisha taka kuwa bidhaa kutapunguza kiwango cha taka nchini, kuongeza ajira pamoja na  kuipunguzia Serikali mzigo wa kutenga maeneo kwa ajili ya kuhifadhia taka kila mara.

Usafi ni kauli mbiu ambayo imeshika kasi awamu hii ya tano ambapo katika sherehe za Uhuru (Tisa Desemba) Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwataka watanzania wote kushiriki usafi maeneo yanayowazunguka na vituo vya jamii kama hospitali, zahanati na vituo vya afya.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!