Sunday, June 12, 2016

Agizo la Waziri mkuu Kassim Majaliwa kwa watendaji wote wa serikali

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji wote wa serikali, walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, maafisa elimu, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, kuhakikisha kwamba michango ya fedha na madawati inayotolewa inawafikia walengwa.


Aidha, kila wilaya ianze mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba upungufu wa madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao, ambapo utendaji wa viongozi wa elimu na serikali katika ngazi mbalimbali utapimwa kutokana na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.

Waziri mkuu ametoa wito huo wakati wa matembezi ya hisani ya kukusanya fedha kwaajili ya ununuzi wa madawati kama sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa benki kuu ya Tanzania (BOT) ambapo jumla ya shilingi milioni 273 zimekusanywa na kukabidhiwa kwa waziri mkuu katika matembezi hayo ya hisani.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, gavana wa benki kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndullu, amesema fedha hizo zimetokana na mchango wa BOT milioni 167, michango ya wafanyakazi wa BOT milioni 30 pamoja na michango ya Taasisi za fedha milioni 22 na makampuni ya simu milioni 54, zikilenga kununua madawati yatakayosambazwa kwenye shule zenye upungufu na zisizo na madawati kabisa.

Benki kuu ya Tanzania (BOT) ilianza kutoa huduma kwa wananchi mnamo tarehe 14 Juni mwaka 1996, ambapo mwezi huu benki hiyo inatimiza miaka hamsini ambapo yameshuhudiwa mabadiliko mbalimbali katika uchumi wa taifa, changamoto na mafanikio, aidha katika kipindi hicho taasisi hiyo imetoa mchango wake stahiki kwa maendeleo ya taifa.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!