Wednesday, June 22, 2016

Al-Shabaab yaua Maafisa watano wa Polisi nchini Kenya


MAOFISA watano wa polisi wa Kenya wameuawa mapema jana mjini Mandera katika shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab kutoka Somalia.

Kamishna wa jimbo hilo la kaskazini mashariki mwa Kenya, Job Borongo, amethibitisha wapiganaji hao walifanya shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa magari ya polisi uliokuwa ukielekea El Wak wakitumia guruneti.

Wakati maofisa wanne wakijeruhiwa vibaya, watano waliuawa papo hapo huku gari walilokuwa wakisafiria likiharibiwa.

Msafara huo wa polisi ulikuwa ukitoa ulinzi kwa msafara wa mabasi ya abiria, utaratibu ulioanzishwa baada ya wapiganaji hao kuteka basi moja na kuua abiria Wakristo 28.

Hata hivyo, Gavana wa Mandera, Ali Roba, aliwalaumu maofisa wa polisi eneo hilo kwa kupuuza tahadhari iliyotolewa na wenyeji kuhusu mashambulio ya kigaidi.

Roba alisema walipuuza vyanzo vya kiintelijensia kuhusu kuonekana kwa wapiganaji hao waliojihami kwa silaha.Hii si mara ya kwanza Mandera kushuhudia mashambulizi kutoka kwa Al-Shabaab.

Shambulizi lake la Novemba 2014 liliwaacha wasafiri wengi wasiokuwa Waislamu na hofu ya kusafiri, na hivyo kuilazimu Serikali kutoa ulinzi kwa mabasi ya uchukuzi wa umma.

Mwezi mmoja baadaye wapiganaji hao waliwaua wachimba madini 36 katika eneo hilo hilo.Kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulizi katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya likitaka kushinikiza taifa hili jirani kuondoa majeshi yake Somalia.

Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi Somalia mwaka 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara nchini hapa.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!