Tuesday, June 21, 2016

Bajeti Kuu Ya Serikali 2016/2017 Yapitishwa Bungeni...licha ya wabunge wa kambi ya upinzani kutoka nje...Mafao ya Viongozi wote Kukatwa Kodi


Serikali ya Tanzania imepitisha bajeti ya shilingi trilion 29.5 kwa kupigiwa kura huku wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika huyo

Katika vikao vya Bunge la 11, wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku 23 sasa kwa madai ya kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa Bunge Dkt.Ackson Tulia.

Wakichangia bajeti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika Bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha katika ofisi ya mkaguzi wa serikali CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na kuachana na mpamgo wa kuanza kuwakata kodi wabunge katika mafao ya kiinua mgongo ya Wabunge, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema msimamo wa serikali upo pale pale.

Kuhusiana na makato ya kodi kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata kodi hiyo kwa viongozi wote wa kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi nchini.

Baadaye jioni wabunge walipiga kura mmoja mmoja kupitisha bajeti hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo bungeni walipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu "Ndiyo" akimaanisha anaipitisha bajeti hiyo.

Akitangaza matokeo ya kura baada ya wabunge kuipigia kura Bajeti hiyo Bungeni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah amesema Idadi ya wabunge wote waliokuwepo ukumbini ilikuwa 252 ambapo kati yao waliopiga kura za ndiyo walikuwa 251 huku kukiwa hakuna kura ya hapana.

Aidha, kura moja ambayo haikupigwa ilikuwa kura ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ambayo kwa kawaida huwa ni kura ya maamuzi.

Dk. Kashilillah amesema idadi ya wabunge wote Kikatiba ni 393 lakini hadi sasa wabunge waliopo ni 389 huku wabunge 137 walikuwa hawapo ukumbini.

Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Naibu Spika amesema Bajeti hiyo imepitishwa kwa kishindo kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, akidi ya kikao cha Bunge kuendelea ni nusu ya wabunge ambao ni 195 na ili Bajeti hiyo ipitishwe ilitakiwa kupigiwa kura ya ndiyo na nusu ya akidi ya wabunge 195 ambao ni wabunge 98.

Upitishwaji wa Bajeti hiyo ni umefanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 107 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo inaelekeza kwamba mjadala kuhusu Hotuba ya Bajeti utakapomalizika huku Kanuni ya 77 (1) ikieleza idadi ya wabunge wakati wa kufanya maamuzi kwamba itakuwa ni nusu ya wabunge wote.

Wakati huohuo Bunge limepitia Muswada wa Sheria ya kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa mwaka 2016.Muswada huo umepitishwa leo katika hatua zake zote mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali.

Akielezea namna ya upitishwaji wa Muswada huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amesema ni tofauti na miswada mingine kwa kuwa hautangazwi katika Gazeti la Serikali na wala haujadiliwi na wabunge.

Mapema Asubuhi mara baada ya dua, wabunge wa upinzani waliziba midomo yao kwa karatasi na Plasta na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.

Mbunge wa Vunjo Kupitia chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. James Mbatia kwa niaba ya wabunge hao amesema hawataacha kulalamikia ukiukwaji wa sheria unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.

Baadhi ya wabunge wa Vyama vya Upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo Tangu Mei 30 mwaka huu.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!