Saturday, June 4, 2016

Bunge la Afrika Mashariki Lapitisha Bajeti ya mwaka 2016/17 ya Sh. bilioni 210


BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limepitisha bajeti yake ya mwaka 2016/17 ya Dola za Marekani milioni 100.1 (Sh bilioni 210) ikiwa ni pungufu ya asilimia 10 ya bajeti ya mwaka jana wa 2015/16 ambayo ilikuwa ni Dola za Marekani milioni 111 (Sh bilioni 233).

Aidha, kupungua kwa bajeti hiyo kumetokana na baadhi ya wahisani kupunguza misaada yao kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (ECA) huku nchi wanachama zikishindwa kuchangia kikamilifu na ni nchi moja tu ya Kenya ndiyo mpaka sasa imeweza kuchangia kwa asilimia 100.

Akizungumza jana baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa EALA, Abdullah Mwinyi wa Tanzania alisema kupungukiwa kwa asilimia kumi ya bajeti ni pigo kubwa, hivyo wamejipanga vizuri kujitegemea katika bajeti hiyo kulingana na kiasi walichonacho kwa kubuni njia bora za mapato.

Hata hivyo, alisema licha ya changamoto hizo nchi wanachama zimekuwa tatizo kubwa kwa kutotimiza ahadi zao kikamilifu za kutoa fedha kwa wakati na pia kuwepo kwa nchi ya Sudan Kusini ambayo imejiunga katika Jumuiya na nchi ya Burundi ambayo imekuwa na migogoro ya kisiasa suala ambalo linaongeza changamoto katika Jumuiya hiyo.

Naye Spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega wa Uganda, alisema Bunge limepunguza bajeti kutokana na nchi wanachama kushindwa kuchangia kwa wakati na wafadhili kupunguza bajeti yao ya utoaji misaada yao.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!