Thursday, June 16, 2016

Dr.Bana Amtetea Kikwete Kuhusu Mchakato wa Katiba...Apinga Kikwete Kupelekwa Mhakamani

WASOMI wamesema kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alistahili kupongezwa kwa kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.


Wasomi hao wametoa maoni hayo baada ya mwanaharakati, Jenerali Ulimwengu kusema juzi kuwa Kikwete anapaswa kushtakiwa kama viongozi wengine walioisababishia hasara Serikali. Wasomi wametafsiri maoni hayo ya Ulimwengu kuwa hayakuwa ya kichambuzi, bali ya kiunaharakati.

Akizungumza katika Tamasha la Nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juzi, Ulimwengu alisema Kikwete anastahili kushtakiwa kwa kuwa fedha nyingi zimepotea wakati wa kuunda Katiba Mpya, ambayo haikupatikana.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana , alisema anamheshimu Ulimwengu kama mchambuzi wa kimtazamo, lakini katika suala hilo hakuwa sahihi.

“Ulimwengu ni kati ya watu kumi kwa mitazamo ya kimsimamo na wachambuzi wazuri lakini katika hili nadhani maoni yake yalikuwa ya kiuanaharakati zaidi na sio ya kichambuzi makini kama tulivyomzoea,” alisema Dk Bana.

Alisema mchakato wa Katiba, ulienda kwa mujibu wa sheria na Bunge ndiyo lenye dhamana ya kutunga sheria na siyo Rais huyo mstaafu, ambaye yeye alianzisha tu na kwamba Kikwete alifanya kila njia, kuhakikisha anawaridhisha watanzania kupata katiba.

Hata hivyo, alisema Watanzania wanatakiwa kumpongeza Kikwete kwa kuanzisha mchakato wa Katiba kuliko kuwa na mawazo kwamba anastahili kupelekwa mahakamani.

“Bunge lile la Katiba lilijadili na kufikia lilipofikia na katiba iko uwanjani, tunachosubiri ni kupiga kura ya maoni, Kikwete kosa lake nini? Mchakato ule ulikuwa wa Watanzania wote na siyo wa Kikwete,” alisema Dk Bana.

==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!