Friday, June 17, 2016

Kamati kuu ya CCM Kukutana Kesho Jijini Dar


KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatarajia kukutana Kesho jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo itakutana chini ya Mwenyekiti wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambapo miongoni mwa wajumbe watakaoingia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein na Rais John Magufuli.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ilisema kikao hicho ni miongoni mwa vikao vya kawaida vya chama hicho.

Kikao hicho cha Kamati Kuu kinakutana, ikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, unaotarajia kufanyika mjini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine, utatumika na Mwenyekiti wa sasa Jakaya Kikwete kukabidhi wadhifa huo kwa mrithi wake, Rais Magufuli.

Hivyo kikao hicho cha kesho, licha ya kuwa hazijawekwa wazi ajenda zitakazojadiliwa, lakini ajenda ya maandalizi ya mkutano huo mkuu huenda ikawa ni miongoni mwa ajenda muhimu zitakazojadiliwa na Kamati Kuu.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka amekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana, ikimhusisha na kueleza kuwa CCM imetoa taarifa ya kukanusha madai ya hivi karibuni yaliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

“Hiyo taarifa siyo ya kwangu (Sendeka) wala siyo ya Chama Cha Mapinduzi…ni taarifa ambayo haikutolewa na mimi wala na chama chetu,” alisema Sendeka
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!