Friday, June 3, 2016

Majengo 15 ya Polisi kujengwa nchini


SERIKALI inajiandaa kutumia Sh bilioni moja katika ujenzi wa kila jengo moja la Kamanda wa Polisi ili kukidhi mahitaji ya majengo 15 ya makamanda hao nchi nzima. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusufu Masauni alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Musa Ntimizi (CCM).

Ntimizi katika swali lake, alisema mazingira ya makazi ya polisi katika Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Uyui, Isikizya ni magumu kwa sasa ambapo askari wanaishi katika nyumba za kupanga na katika mabanda ya mabati, yaliyojengwa karibu na kituo.
 
Kutokana na hali hiyo, alitaka serikali ieleze ina mpango gani wa kuboresha mazingira hayo kwa askari wetu, ili wafanye kazi katika mazingira bora zaidi. Akijibu swali hilo, Masauni alisema ujenzi wa vituo vya Polisi, majengo ya utawala na nyumba za kuishi askari, ni suala linalohitaji fedha nyingi kwa nchi nzima.

Alisema kwa sasa kuna upungufu katika vituo vya Polisi daraja A na Daraja B, ambavyo ni vituo vinavyotakiwa kujengwa katika makao makuu ya wilaya na mikoa ya kipolisi na katika miji inayokua.

Kwa mujibu wa Masauni, vituo vya daraja A vinavyotakiwa kujengwa nchi nzima ni 94, kwa wastani wa Sh bilioni 94 na vituo daraja B vinahitajika 382, kwa gharama ya Sh bilioni 191 na vituo Daraja C vinavyohitajika 4,043 kwa gharama ya Sh bilioni 950.

Mbali na vituo hivyo, Masauni alisema pia kuna mahitaji ya nyumba za kuishi askari 35,000 ambazo ujenzi wake umekadiriwa kutumia Sh trilioni 2.8. Kutokana na hali hiyo, Masauni alisema kila mwaka Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 3,500 nchi nzima.

Pia alisema Serikali ya Awamu ya Tano, ina mpango wa kujenga nyumba nyingine 4,136 kutokana na mkopo wa dola za Marekani milioni 500 kutoka nchini China na tayari mpango huo upo Wizara ya Fedha na Mipango.

Kuhusu ujenzi wa vituo vya Polisi Daraja A, B na C na majengo ya makamanda, Serikali itaendelea kujenga kulingana na uwezo wa upatikanaji fedha. Alisema pia wizara yake, itaendelea kuwasiliana na serikali za mitaa, ili panapoanzishwa wilaya na mikoa, kuwepo na huduma zinazohusu ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya Polisi na nyumba za kuishi askari.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!