Tuesday, June 14, 2016

Mvutano Wabunge Upinzani, CCM Waibukia Kwenye Semina

MVUTANO kuhusu uendeshaji wa Bunge unaoendelea kati ya wabunge wa CCM na wa vyama vya upinzani, umeibukia kwenye semina za mafunzo ya wabunge, baada ya wabunge wawili kutoka vyama tofauti kuonesha tofauti zao kisiasa.


Hali hiyo ilijitokeza kwenye semina kuhusu mbinu za wabunge kufuatilia matumizi ya fedha za umma, ambayo miongoni mwa watoa mada alikuwa Dk Colman Msoka, kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mvutano huo uliibuka kati ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako (CCM) wakati wakichangia mada mbalimbali zilizotolewa kuhusu ufuatiliaji wa matumizi ya Serikali. Akichangia, Selasini alisimama na kusema Bunge la sasa limegeuka mhuri wa kupitisha kila kitu kutoka serikalini.

Akitumia uzoefu wake kuwa mbunge wa vipindi viwili, kwa maana ya 2010-2015 na sasa 2015-2020; Selasini aliwaambia wabunge hasa walio wapya kuwa anaona tofauti kubwa ya Bunge lililopita na la sasa. “Tukazanie kuimarishwa kwa demokrasia ya Bunge la sivyo tunakokwenda Bunge litafutika…mimi ni mbunge wa vipindi viwili, naweza kufananisha Bunge lililopita na hali ilivyo katika Bunge la sasa,…la sasa ni mhuri,” alidai.

Alidai kuwa wakati kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali, kinachoonekana kwa sasa wabunge wanaiogopa. Alisema kama hali hiyo itaendelea, hakuna haja ya wao kuendelea kuwa wabunge. Kwa mujibu wa Selasini, katika uandaaji wa bajeti, wataalamu hasa wa Hazina wamekuwa wakijiona ndio wenye uwezo kuliko wabunge na kwamba ndio maana hawachukui maoni yao.

Kauli hiyo ya Selasini ilimuinua Nsanzugwako, ambaye alimtaka mbunge huyo wa Chadema aache kupotosha wabunge wapya akisema wabunge ni zao la vyama vya siasa na vyama vya upinzani vina majukumu tofauti na chama tawala. Nsanzugwako ambaye hii ni mara yake ya pili kuwa Mbunge, alisema vyama vya upinzani vilishindwa katika uchaguzi mkuu, hivyo havina ajenda lakini vina kazi ya kufanya ambayo ni kukosoa Serikali.

Alisisitiza umuhimu wa chama tawala kupewa nafasi ya kutekeleza ajenda yake kwa kuwa ndio kilichoshinda Uchaguzi Mkuu. Alishauri kuandaliwe pia mafunzo kuhusu kazi za chama chenye Serikali na chama cha upinzani. Kuhusu kuimarisha kazi ya Bunge katika usimamizi wa Serikali, Nsanzugwako aliwataka wabunge kujenga uhusiano bila kujali vyama uwawezeshe kufanya kazi ya Bunge.

Alihadharisha kuwa bila uhusiano wa wabunge katika ufuatiliaji wa bajeti, wataishia kutunishiana misuli bungeni kati ya chama tawala na vyama vya upinzani. Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilaly (CCM), alisema kamati anayoiongoza na Bunge kwa ujumla, haviwezi kushikiliwa na Serikali.

Alisema ili kuimarisha kamati ambazo zinategemewa kutoa taarifa kwa Bunge, chombo hicho kiliona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo wabunge waelewe umuhimu wao katika kufuatilia bajeti ya Serikali. Aeshi alisema kama Kamati ya Bunge ikiwa dhaifu na Bunge litakuwa dhaifu kwa kuwa itapeleka taarifa dhaifu na kufanya Bunge kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Alisema ndiyo maana mafunzo hayo yamehusisha wajumbe wa PAC, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Akizungumza katika mafunzo hayo, mmoja wa watoa mada, Dk Msoka, kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema utafiti umeonesha kuwa kamati za Bunge zinapokuwa madhubuti, pia Bunge huwa madhubuti.

Wakati huo huo, Bunge linaendelea leo, ambapo baada ya maswali na majibu wabunge wataendelea kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Serikali na kutoa maoni kuhusu Mpango wa Serikali wa 2016/2017.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!