Wednesday, June 15, 2016

Naibu Spika Atolea Ufafanuzi Kuhusu Sakata la Wapinzani


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amelazimika kutolea ufafanuzi sakata la wabunge wa upinzani kutoka nje ya bunge.
Dkt Tulia ametoa ufafanuzi baada ya hoja hiyo kuibuliwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wakichangia mjadala wa bajeti katika kikao cha 42 mkutano wa 3.

Baadhi ya wabunge waliogusia suala hilo ni Livingston Lusinde pamoja na Daniel Nsazugwako ambao wameelezea kuwa wabunge hao wanataka kurudi bungeni na kumuomba Naibu Spika kuwasamehe.

Baada ya hoja hizo kuibuliwa ndipo Naibu Spika akalieleza bunge kuwa hakuwatoa yeye bungeni wabunge hao na badala yake alieleza kinachoendelea kuhusu wabunge hao ambao wameendelea kutoka nje kila mara ambapo vikao vya bunge vinapoongozwa na Naibu Spika.

Katika ufafanuzi wake, Dkt Tulia amesema kuwa wapinzani tayari wamekwisha peleka hoja kwa Spika ya kutokuwa na imani na Naibu Spika kwa mujibu wa kanuni ya 138, na kuongeza kuwa kanuni hizo hizo haziwapi haki ya kususia vikao, hivyo hana la kufanya hivi sasa zaidi ya kusubiri maamuzi ya Spika.

"Wapinzani wamepeleka hoja kwa Spika kwa mujibu wa kanuni ya 138, na ni haki yao, lakini suala la kutokuwa na imani siyo jipya, hoja kama hiyo imewahi kutolewa siku za nyuma dhidi ya Spika Makinda lakini hawakususia vikao, na hizo kanuni haziruhusu, katika kanuni hizi hakuna sehemu yoyote inayoruhusu wabunge kususia vikao" Amesema Dkt Tulia.

Aidha katika hatua nyingine wabunge wameendelea kutaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ) aongezewe bajeti ili aendelee kuwa na uwezo mkubwa katika kudhibiti hesabu za serikali.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!