Saturday, June 4, 2016

Paul Makonda aomba Boti za Kivita kutoka China Kusaidia Ulinzi


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameomba boti za kivita kutoka nchini China ili kusaidia ulinzi katika ukanda wa bahari ya Hindi.

Aliomba boti hizo Dar es Salaam jana wakati alipotembelea boti ya Jeshi la Wanamaji kutoka China waliokuja nchini kwa ziara ya kirafiki wakiwa wametoka kutekeleza jukumu la kushiriki katika ulinzi katika Ghuba ya Aden.

Alisema upatikanaji wa boti hizo utasaidia kudhibiti wanaoingiza na kushusha mizigo kwa njia wa magendo sambamba na wanaovamia watu na kupora mali za watu katika fukwe hapa nchini.

Makonda alisema kuna nyumba zilizo kama maghala ambayo hayafunguliwi mchana, yanaingiza mizigo usiku na kuisababishia serikali hasara kwa kutoingiza kodi, hivyo boti hizo zitakazokuwa za kisasa zitakuwa msaada mkubwa kwa Polisi katika Kanda ya Dar es Salaam, kufanya ukaguzi katika ukanda wa bahari ya Hindi.

Naomba mtusaidie boti kama tatu au nne ambazo tunaamini zitasaidia kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha vitendo vya uhalifu katika bahari unatoweka kabisa,” alisisitiza.

Alisema pia serikali ya mkoa imezungumza na Balozi wa China nchini kuhusu kuanzishwa kwa kituo kitakachofundisha polisi 300 watakaokuwa na uwezo wa kufika sehemu yoyote ya mkoa linapotokea tukio ndani ya dakika tano.

Alisema kuanza kwa mpango huo mkoa utakuwa wa kwanza kwa Bara la Afrika kuwa na askari wa aina hiyo, hivyo serikali ina wajibu wa kulishughulikia na kufanikisha mchakato huo kwa askari wa nchi kavu na hata majini.

Mkuu wa Tawi la Mipango la Maendeleo Jeshini, Meja Jenerali Simon Mumwi alisema ziara hiyo itawasaidia kubadilishana uzoefu na wanamaji kutoka nchini kwao na taarifa mbalimbali huku akiahidi kudhibiti wa matukio ya kihalifu, hasa katika ukanda wa bahari.

Niseme tu bahari yetu ni salama na jeshi la wanamaji lipo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi,” alisema Mumwi.Balozi wa China nchini, Lu Youqing alisema ujio wa meli hiyo ni ishara ya njema ya mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya China na Tanzania uliodumu tangu enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!