Monday, June 13, 2016

Serikali yatenga Sh.bilioni 59.5 Kuongeza Mtaji kwa Kila Kijiji Nchini

 
Serikali imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 59. 5 katika Mwaka 2016/17 ili kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
 
Hayo yamesemwa leo Bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenister Mhagama alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Jackiline Ngonyani aliyetaka kujua lini serikali itaanza kutoa kiasi cha Tsh. Milioni 50 kwa kila kijiji au mtaa ili kuwasaidia wananchi kuboresha mitaji yao.
 
“Fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija katika matumizi ya fedha hizo,”alisema Mhagama.
 
Mhagama alimuomba Mbunge huyo kusubiri utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 mara baada ya kukamilika kwa mfumo wa muundo wa Utekelezaji wa zoezi zima ambapo kazi imeanza kufanyika.
 
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayo nia ya dhati ya kuwainua wananchi hasa wa kipato cha chini ili kukuza mitaji yao.
 
“Serikali hii inatekeleza kwa vitendo kile inachokiahidi aliongeza Mhagama na kuwataka waheshimiwa wabunge waeendelee kuiamini Serikalia yao ambayo inafanya kazi kwa dhati kama ilivyo kauli mbiu ya mhe. Rais John Pombe Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!