Tuesday, June 14, 2016

Siku 21 alizotoa Makonda kwa benki zaisha


WAKATI siku 21 zilizotolewa kwa benki zilizokuwa zikitumika kuweka mishahara ya watumishi hewa zikiwa zimeisha jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ameshapata taarifa alizohitaji kutoka katika benki hizo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makonda alisema benki hizo zimeshapeleka taarifa ingawa aliahidi kutoa ufafanuzi zaidi baada ya kukaa na kuzipitia. Makonda alitoa siku hizo 21 zilizoisha jana, benki hizo kurejesha fedha hizo serikalini au zitaje watu waliokuwa wakitumia akaunti husika.

Alichukua hatua hiyo baada ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa na ongezeko kubwa la watumishi hewa ambao fedha walizokuwa wanalipwa zilikuwa zinapita katika benki husika. Mpaka sasa, mkoa wa Dar es Salaam umebainika kuwa na watumishi hewa 283, ambao wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 3.6 ambazo zilitumika kuwalipa mishahara.

Makonda alisema benki ndio pekee wanaoweza kusaidia mkoa, kutambua wahusika waliokuwa wanatumia akaunti hizo pamoja na wale waliokuwa wanachukua fedha hizo. Alitaja benki hizo na fedha zilizoko ni NMB yenye Sh bilioni mbili, CRDB zaidi ya Sh milioni 400, NBC zaidi ya Sh milioni 141, DCB Sh milioni 85, Standard Chartered zaidi ya Sh milioni mbili na Community Benki zaidi ya Sh milioni 100.

“Hakuna mtu anayeweza kutumia akaunti ya mtu bila kufuata taratibu za kibenki, hata kama mtu amefariki kuna taratibu za kufuata ndipo apate akaunti, naamini benki hizi zitasaidia kuwatambua wahusika wote,” alisisitiza.

Wakati huo huo gazeti hili lilizungumza na wasemaji wa baadhi ya benki hizo ambao wengi walisema mwenye uwezo wa kutolea ufafanuzi ni Mkuu wa Mkoa. Meneja Uhusiano wa NMB, Vicent Mnyanyika alisema wao kama benki hawawezi kusema chochote ni vyema suala hilo likatolewa ufafanuzi na Makonda ambaye ndio aliyeagiza kama amepata mrejesho kutoka katika benki hizo.

Kwa upande wa CRDB, Meneja Uhusiano wa Benki hiyo, Godwin Semunyu alisema, Mkurungenzi Mtendaji wa benki hiyo ndiye atatolea ufafanuzi.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!