Wednesday, June 15, 2016

Ukweli Afya ya Spika Job Ndugai

KUFUATIA uvumi wa mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii juu ya kufariki dunia kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, Risasi Mchanganyiko limetafuta na kufanikiwa kupata ukweli juu ya afya ya kiongozi huyo mkuu wa wabunge Tanzania.
Awali, kulikuwa na taarifa katika mitandao ya kijamii, ikitoa madai hayo, hasa kutokana na kutoonekana kwa muda mrefu kwa Spika akiongoza vikao vya Bunge vinavyoendelea kujadili bajeti kuu ya serikali mjini Dodoma.

Kutotolewa kwa maendeleo ya afya yake ndilo jambo linalowafanya wengi kuziamini taarifa hizo za mitandaoni na hivyo kupiga simu chumba cha habari kutaka kujua uhakika wake hasa kwa kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa Spika kwenda nchini humo kuangaliwa afya yake.

Gazeti hili lilimtafuta Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah ili kupata ufafanuzi wa taarifa za mitandao zilizokuwa zikitembea juzi (Jumatatu) kuwa mbunge huyo wa jimbo la Kongwa mkoani Dodoma amefariki, lakini simu yake haikupo-kelewa.

Lakini Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipatikana na kuhusu ‘ishu’ hiyo, alisema ingawa alikuwa Dar es Salaam, anavyofahamu ofisi ya mhimili huo wa dola, haina taarifa tofauti na zilizotolewa awali.

“Watu bwana sijui wakoje, mimi huu uvumi niliusikia, lakini afya ya Spika ni nzuri na anaendelea na uchunguzi wa afya yake kama kawaida,” alisema.

Juni 8 mwaka huu, ofisi ya Bunge ilitoa taarifa rasmi za kukanusha uvumi huo, ikidai hali ya mbunge huyo inaendelea vizuri katika hospitali anayotibiwa nchini India.

Taarifa hiyo iliwataka watu kupuuza uvumi huo unaowapa hofu wananchi na viongozi, kwani yupo huko akiangaliwa afya yake, kama alivyotakiwa kufanya hivyo na daktari wake mapema mwaka huu.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!