Wednesday, June 15, 2016

Ushahidi wa Jerry Silaa Utata Mahakamani Leo

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo imekwama kufikia uamuzi kutokana na ushahidi wa Jerry Silaa kuwa na utata, anaandika Faki Sosi.
Dk. Onesmo Kyuka, Wakili wa Serikali ameieleza mahakama kuwa, kwa mujibu wa kanuni 21A(2) ya ushahidi, Silaa hana sifa ya kuwa shahidi wa kesi aliyofungua mwenyewe.

Silaa, aliyekuwa mgombea ubunge kwenye Jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam kupitia CCM alifungua kesi hiyo kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Mwita Waitara (Chadema).

Kesi hiyo imesikilizwa katika mahakama hiyo mbele ya Fatuma Mseng ambapo Silaa alifika kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Dk. Kyuka ameieleza mahakama kuwa, utoaji ushahidi mahakamani lazima kuzingatiwe sheria na kwamba, Silaa hakuenda kwa msajili wa mahakama kwa hatua za awali za ushahidi.

Akitoa utetezi wake Masumbuko Lamwai, Wakili wa Silaa amesema kuwa, bado kuna haja ya mahakama kukubali ushidi huo kutokana na Silaa kuhusika kwake.

Madai ya Silaa katika shauri hilo ni kuwa, matokeo ya uchaguzi yalitangazwa tarehe 28 Oktaba saa 10 alfajiri mwaka jana ambapo yeye alipewa hati tofauti ya matokeo halisi.

Uamuzi kuhusu nafasi ya Silaa kuwa shahidi kwenye kesi hiyo utatolewa kesho.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!