Wednesday, June 15, 2016

Wadau wa Elimu Kumwaga Bilioni 75/- Stadi za KKK


MAFANIKIO yaliyoonekana katika programu ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa madarasa ya chini, yamewavutia wadau mbalimbali wa elimu na kuahidi kutoa Sh bilioni 75 kwa ajili ya kuimarisha stadi hizo.

Akizindua taarifa ya kupima uwezo wa watoto kupitia programu hiyo Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema utafiti uliofanywa mwaka huu umeonesha kuwa, uwezo wa watoto katika mambo hayo matatu unaonekana kukua katika viwango tofauti kiasi cha kuridhisha.

Aliongeza kuwa, stadi hiyo ilifanyika katika shule 650 nchini na kujumuisha watoto 7,000 ambapo baada ya uzinduzi huo, taarifa hiyo itachambuliwa zaidi na wataalamu ili kuongeza mafanikio zaidi katika mambo hayo.

Alisema wakati inaanza programu ya Matokeo Makubwa Sasa, ilionekana suala la watoto kutojua kusoma, kuhesabu na kuandika ni tatizo kubwa, hivyo ikawekwa mikakati ya kuongeza ufundishaji kuondokana na tatizo hilo.

Mkakati wa Serikali ni kuinua ubora wa elimu ambapo itajenga misingi mizuri zaidi na kwamba tayari wamechapisha vitabu vitakavyosambazwa nchi nzima na pia itatoa mafunzo kwa wakaguzi wa elimu, walimu na waratibu wa elimu.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Research Triangle International (RTI) wakishirikiana na Data Vision, kwa msaada wa USAID watoto wa kike wameonekana kufanya vizuri zaidi ya wenzao wa kiume.
==
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Ubuyu Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako, Matusi Hapana!